Genesis 28

1Basi Isaka akamwita Yakobo, akambariki na akamwamuru, akisema, “Usioe mwanamke wa Kikanaani. 2Nenda mara moja mpaka Padan-Aramu, kwenye nyumba ya Bethueli baba wa mama yako. Uchukue mke kati ya binti za Labani ambaye ni ndugu wa mama yako. 3Mwenyezi Mungu
Mwenyezi Mungu hapa ni jina la Kiebrania, El-Shaddai (yaani Mungu Mwenye utoshelevu wote).
na akubariki uwe na uzao uongezeke idadi yako upate kuwa jamii kubwa ya watu.
4Na akupe wewe na uzao wako baraka aliyopewa Ibrahimu, upate kumiliki nchi unayoishi sasa kama mgeni, nchi ambayo Mungu alimpa Ibrahimu.” 5Kisha Isaka akamuaga Yakobo, naye akaenda Padan-Aramu, kwa Labani mwana wa Bethueli Mwaramu, ndugu wa Rebeka, aliyekuwa mama wa Yakobo na Esau.

6Sasa Esau akajua kuwa Isaka amembariki Yakobo na kumtuma kwenda Padan-Aramu ili achukue mke huko na kwamba alipombariki alimwamuru akisema, “Usioe mke katika binti za Wakanaani,” 7tena kwamba Yakobo amewatii baba yake na mama yake naye amekwenda Padan-Aramu. 8Esau akatambua jinsi ambavyo baba yake Isaka anavyowachukia binti za Wakanaani. 9Ndipo Esau akaenda kwa Ishmaeli, akamwoa Mahalati, ndugu wa Nebayothi na binti wa Ishmaeli mwana wa Ibrahimu, kuongezea wale wake wengine aliokuwa nao.

Ndoto Ya Yakobo Huko Betheli

10Yakobo akatoka Beer-Sheba kwenda Harani. 11Alipofika mahali fulani, akalala hapo kwa sababu jua lilikuwa limetua. Akachukua jiwe moja la mahali pale, akaliweka chini ya kichwa chake akajinyoosha akalala usingizi. 12Akaota ndoto ambayo aliona ngazi imesimamishwa juu ya ardhi, ncha yake ikiwa imefika mbinguni na malaika wa Mungu wakawa wakipanda na kushuka juu yake. 13Juu yake alisimama Bwana, akasema, “Mimi ni Bwana, Mungu wa baba yako Ibrahimu na Mungu wa Isaka. Nchi ambayo umelala juu yake, nitakupa wewe na uzao wako. 14Uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi na mashariki, kaskazini na kusini. Kupitia wewe na uzao wako mataifa yote ya duniani yatabarikiwa. 15Niko pamoja nawe nami nitakulinda kila uendako na nitakurudisha katika nchi hii. Sitakuacha mpaka nitakapofanya hayo niliyokuahidi.”

16Yakobo alipoamka kutoka usingizini, akawaza, “Hakika Bwana yuko mahali hapa, wala mimi sikujua.” 17Kwa hiyo akaogopa, akasema, “Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka hapa ndipo nyumba ya Mungu ilipo, hili ni lango la mbinguni.”

18Asubuhi yake na mapema, Yakobo akalichukua lile jiwe aliloliweka chini ya kichwa chake, akalisimamisha kama nguzo na kumimina mafuta juu yake. 19Mahali pale akapaita Betheli,
Betheli maana yake Nyumba ya Mungu.
ingawa mji ule hapo kwanza uliitwa Luzu.

20Kisha Yakobo akaweka nadhiri, akisema, “Kama Mungu akiwa pamoja nami na kunilinda katika safari niendayo, akinipa chakula nile na nguo nivae 21na nirudi salama nyumbani kwa baba yangu, hapo ndipo Bwana atakuwa Mungu wangu, 22nalo jiwe hili nililolisimamisha kama nguzo litakuwa nyumba ya Mungu na katika yote utakayonipa nitakutolea wewe sehemu ya kumi.”
Copyright information for SwhKC